Alibaba

vendredi 10 mai 2013

BI KIDUDE KAFA FUKARA

KUSOMA HABARI ZOTE BOFYA HAPA
Stori; Imelda Mtema
MAISHA ya mwisho ya mwanamuziki maarufu wa taarab na fundi wa kufunda unyago nchini, Fatma binti Baraka ‘Bi Kidude’ hakika yalitia simanzi, Ijumaa Wikienda lina ripoti ya kuumiza moyo.
Bi Kidude na Matalii
Bi Kidude, pamoja na kutamba kwa nyimbo zake na kufanya ziara za mara kwa mara sehemu mbalimbali duniani, amekufa akiwa fukara huku watu wachache wakinufaika kwa kipaji chake cha uimbaji.
Dirisha la kwanza kushoto ndio chumba achokuwa akilala...
WAOMBOLEZAJI WAMWAGA MACHOZI
Baadhi ya waombolezaji waliofika nyumbani kwake, Raha Leo mjini Unguja kwa ajili ya kumsitiri, walimwaga machozi pale walipokutana na hali duni ya maisha ya mwanamuziki huyo mkongwe.
Godoro alilokuwa akilalia Bi kidude likiwa limetupwa nje

GODORO CHAKAVU
Mwandishi wa gazeti hili aliyekuwa Zanzibar alipata fursa ya kuyaona mazingira aliyokuwa akiishi mwanamuziki huyo, hakika ilitia uchungu.
Bi Kidude ambaye alifanya ziara nyingi za kimataifa, alikuwa akilalia godoro chakavu lililotoboka na kutawaliwa na uchafu katika kila pembe.
GODORO LATUPWA
Godoro hilo, ilibidi litupwe baada ya kifo chake ili waombolezaji wengine wasilione na kubaini ukweli wa maisha duni ya Bi Kidude ambaye alifariki dunia Aprili 17, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 104.
Mbali na godoro, chumba cha Bi Kidude hakikuwa na hadhi yake, kilikuwa kichafu na kulazimika kusafishwa haraka ili kusitiri aibu ya marehemu ambayo ilisababishwa na watu waliokuwa wakimtumia kuchuma fedha kwa mgongo wake.

WATU WALIKUWA WAKIMCHUNGULIA
Jambo la kushangaza ni kwamba hadi anaaga dunia Jumatano iliyopita na kuzikwa kesho yake, nyumba ya Bi Kidude haikuwa imemalizika kujengwa.
Nyumba hiyo ilikuwa imekamilika upande mmoja tu bila ya kujua fedha za shoo na matamasha mbalimbali makubwa alizokuwa akizipata zilikuwa zikienda wapi.
Dirisha la chumba chake wavu ulikuwa umekatika na kufanya mbu wa kumwaga kujazana chumbani mwake huku vibaka na watu wengine wasio na tabia njema kuweza kumchungulia akiwa ndani wakati wa usiku.

ALIKUWA KAMA OMBAOMBA
Enzi za uhai wake, waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali duniani na watalii walipomtembelea Bi Kidude, kitu cha kwanza aliwaomba fedha za kununulia sigara hivyo kuonekana kama ombaomba.
Mbali na fedha za sigara pia angeweza kuomba kiasi kingine cha fedha kwa ajili ya matumizi yake mengine.

TATIZO NI NINI?
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, mtoto wa kaka wa marehemu Bi Kidude, Baraka Othuman Baraka alikiri kwamba shangazi yake alikufa akiwa hohehahe.

ELIMU YATAJWA
“Udhaifu wa kwanza ambao watu wengi hasa waandaaji wa matamasha makubwa ndani na nje ya nchi walioutumia kuvuna fedha za Bi kidude ni elimu kwani hakwenda shule zaidi ya Madrasa,” alisema Baraka.
Baraka alisema kuwa watu wengi walipata mwanya huo na kumtumia shangazi yake na kisha kumuacha fukara bila ya kumwachia faida yoyote.
“Wewe umesema nyumba haijamaliziwa, hebu angalia hata upande ulioisha haujapigwa hata plasta,” alisema Baraka kwa majonzi.
Baraka aliongeza kuwa kitu ambacho kinamuumiza ni kuona Bi Kidude amekuwa akifanya matamasha ya ndani na nje lakini maisha yake yaliendelea kuwa duni.
“Watu walimtapeli sana Bi Kidude, kuna waliokuwa wakimfanyisha matamasha kila mwaka, Bi Kidude alikuwa akienda kushinda ofisini kwao ili wampatie fedha za kununulia godoro, nao wakawa wanamuahidi kwamba watampa lakini mpaka anafariki dunia hakuambulia chochote,” alisema Baraka.

MATIBABU DUNI
Baraka ameliambia Ijumaa Wikienda kwamba, ndugu walikuwa wakihangaika na Bi Kidude katika hospitali za kawaida tu pale alipoumwa, wala hawakuwahi kupata msaada mkubwa wa matibabu pamoja na kwamba alikuwa kama nembo ya Zanzibar.
“Wageni wengi waliokuwa wakija Zanzibar walikuwa wakitaka kumuona Bi Kidude, lakini ndiyo hivyo hakuna aliyemjali katika suala la matibabu,” alisema Baraka.
Pamoja na  lawama hizo, Baraka alimshukuru Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein ambaye aliwahi kumtembelea marehemu na kumuachia kiasi cha fedha wakati wa Sikukuu ya Eid El Fitr.

LAWAMA ZA NDUGU?
Watu wengi msibani walitupa lawama kwa ndugu wa marehemu kutokana na kutomwangalia kwa karibu na kuratibu shughuli zake za muziki, Baraka anasemaje?
“Kila ndugu tulipojaribu kutaka kuingilia kati juu ya maslahi ya marehemu tulionekana viherehere, baadhi ya watu walikuwa wakituona kama vile tunawabana na kuanza kutoa shutuma kwetu,” alisema.

FEDHA ZAKE ZAYEYUKA BENKI
Kama vile haitoshi, Baraka alidai kwamba kuna watu walijidai kwamba walikuwa wakimwekea Bi Kidude fedha benki lakini kila walipowauliza ilikuwa ni ugomvi hivyo mbali na nyumba kuukuu aliyokuwa akiishi, hakuna utajiri wowote alioacha hivyo ni changamoto kwa wasanii wa Kibongo.
“Sijui hizo fedha kama zipo kweli na hata zikiwepo zitasaidia nini wakati mtu mwenyewe ameshafariki?” alihoji kwa hasira.

NENO LA IJUMAA WIKIENDA
Watu wengi wanatajwa kuhusika kumhujumu mkongwe huyo kwa kumfanyisha kazi bila malipo, ni rai yetu kuwa wahusika watapeleka kiasi cha fedha walichonacho katika familia yake. 

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire