Google tag

vendredi 9 septembre 2016

KUCHINJA KWA AJILI YA IDDI AL-ADH-HAA.

SUALI
*Nataka kuchinja udh-hiya, lakini sijui wakati gani nichinje na vipi namna na kutoa sadaka hiyo au haina masharti yoyote❓*

JAWABU:

_Kwa hakika kuchinja Udh-hiyah kuna fadhila kubwa sana ndani yake, kwani ni kuadhimisha matukuzo ya Allah kwa aliyoruzuku katika neema zake za wanyama wa miguu minne, nalo ni alama kubwa ya uchamungu kama alivyobainisha hayo Allah mtukufu, basi Allah mtukufu amemuamrisha Mtume wake S.A.W kwa kumwambia:_

*فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ..*

Basi sali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi.

_Na katika Aya hii tukufu kuna dalili ya wazi kuwa kuchinja sadaka ya Udh-hiya ni baada ya kusali sala ya Iddi, nayo ndiyo aliyosema Mtume S.A.W:_ _((Atakaechinja kabla ya sala huyo amejichinjia kwa nafsi yake, atayechinja baada ya sala huyo amepatia sadaka yake na ameipata Sunna ya Waislamu)) [Bukhari 5556]._

_Na kichinjwa cha Udh-hiya ni katika wanyama wa miguu minne tu, nao ni Ngamia, N`gombe, Mbuzi, na Kondoo, na ufuatao ni ufafanuzi wa umri wa kichinjwa na kwa wanaotoshelezwa,_

*Zingatia kama ifuatavyo:*

Ngamia:
_Uchache mwenye kutosheleza ni aliyetimiza miaka miwili._

*Miaka 2 kwa mtu mmoja.*

*Miaka 3 mpaka miaka 5 kamili kwa watu watano.*

*Zaidi ya miaka 5 na kuendelea kwa watu saba.*

N`gombe:
_Uchache mwenye kutosheleza ni aliyemo katika mwaka wa pili._

*Miaka 2 kwa mtu mmoja.*

*Kuanzia mwaka wa 3 mapa wa 4 ni kwa watu watatu.*

*Akiwa katika mwaka wa 4 kwa watu kwa watano.*

*Zaidi ya miaka 4 na kuendelea watu 7.*

Mbuzi:
_Miaka 2 na kluendelea kwa mtu mmoja._

Kondoo:
_Katimiza mwaka 1 na kuendelea kwa mtu mmoja._

TANBIHI:

_Tukisema kuwa inamtosheleza mtu mmoja makusudio ni yeye na watu wa nyumba yake ikiwa anao, yaani wale walio chini ya matumizi yake ya lazima katika nyumba yake._
_Nyama ya kichinjwa cha udh-hiya kinagawiwa mafungu matatu, fungu la kula mwenyewe mwenye kuhusika na Udh-hiyah, fungu la pili ya limbikiza mwenyewe mwenye kuhusika na Udh-hiyah kwa siku zijazo, na fungu la tatu anatoa sadaka kwa masikini na marafiki na walio wa karibu._
_Asili na ndio Sunna kuwa sadaka ya Udh-hiyah inatekelezwa pale anapoishi mwenyewe mwenye kuhusika na Udh-hiyah, basi mwenye uwezo wa kujikurubisha zaidi kwa Allah anayo pia nafasi nzuri ya kuwachinjia mafakiri wa kiislamu na masikini ikiwa wapo sehemu alipo au wako mbali na pale alipo lakini hayo ni baada ya kuhakikisha asili ya kuchinja yeye mwenyewe au kushirkiana na wengine katika sehemu anayoishi._
_Mwisho tunawatakia siku njema za kumi za mwanzo za mwezi huu wa Dhul-_Hijja na tunakumbusha _kuwa Funga ya Afara ina fadhila kubwa sana pia Allah ametuambia hukusiana na vichinjwa vyetu vya Sadaka ya Udh-hiya:_

((Hazimfikii Allah nyama zake wala damu zake, lakini unamfikia uchamungu wenu, namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Allah kwa alivyo kuongoeni, na WABASHIRIE WENYE KUFANYA MEMA)) [Al-Hajji 37]

_Kwa hakika bishara ya Allah ni kubwa mno katika sadaka hii ya Udh-hiyah, kwa mwenye kukusudia uchamungu._

_Allah atutakabalie mema yetu na atufunikie tuliyoteza na alete taufiqi yake katika yote anayoyaridhia._

Wabillahi Taufiiqi.

_Sheikh Hafidh Al Sawafi._