SOKA maridadi linalochezwa na Pep Guardiola linaanzia mbali. Linaanzia katika masharti magumu ambayo yanawanyima raha wachezaji, lakini hawana budi kuyafuata. Ndio maagizo.
Na sasa imebainika kuwa kocha huyo Mhispaniola amepiga marufuku matumizi ya internet katika eneo la mazoezi ya klabu hiyo.
Guardiola ameruhusu maeneo machache kwenye uwanja wa mazoezi la Manchester City, The City Football Academy kupata internet, lakini amepiga marufuku na kukata mawasiliamo katika maeneo ya ndani kwa ajili ya kuwataka wachezaji wake wazingatie zaidi maelekezo yake.
Beki wa kimataifa wa Argentina, Pablo Zabaleta amedai kwamba Guardiola ameamua kuyafanya maisha yao kuwa magumu katika matumizi ya simu au vifaa vinginevyo vinavyotumia internet kwa ajili ya kuwafanya wazingatie zaidi anachowafundisha.
“Anatulazimisha kula chakula cha asubuhi na cha mchana pamoja klabuni. Internet imekatwa na tunakaa bila ya mawasiliano na watu wa nje. Hatuwezi kutumia 3G,” alisema beki huyo wa kimataifa wa Argentina, ambaye ameendelea kupata namba chini ya Guardiola.
Zabaleta, ambaye alinunuliwa na City mwaka 2008 akitokea Espanyol ya Hispania hata hivyo, amedai kwamba anafurahishwa na mbinu za kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich, aliyetua klabuni hapo msimu huu.
“Siku zote unaota ndoto za kufanya mazoezi chini ya makocha bora na leo nimepata nafasi ya kufanya kazi na mmoja kati ya makocha bora. Kwa kweli unajifunza sana, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuishi. Zaidi ya ufahamu wake wa soka lakini pia mapenzi yake kwa soka,” aliongeza Zabaleta.
Hii ni mara ya pili kwa Guardiola kuonyesha makali yake katika kambi ya mazoezi ya City. Julai mwaka huu wakati City wakiwa katika mazoezi ya maandalizi ya msimu beki wa kushoto wa timu hiyo, Gael Clichy alidai Guardiola alikuwa amepiga marufuku baadhi ya vyakula kwa wachezaji wake.
“Uwanjani na nje ya uwanja kila kitu kinaangaliwa kwa umakini. Kwa mfano, utawasikia makocha wakisema afya ni muhimu. Kwa Guardiola, kama uzito wako ni mkubwa basi haufanyi mazoezi na kikosi cha kwanza.
“Ni kitu ambacho unakisikia sana lakini kwangu ni mara ya kwanza kwa kocha kufanya hivyo. Kwa hiyo kuna wachezaji wachache wa kikosi cha kwanza ambao hawafanyi mazoezi na sisi,” alisema Clichy.
“Kuna juisi ameziondoa katika orodha, Pizza na vyakula vizito.
Kuna watu huwa wanadhani ‘Hilo ni jambo la kawaida na lazima iwe hivyo’ lakini ukweli ni kwamba, sio mara zote mambo yanakuwa hivi. Nimekuwa katika mpira kwa muda mrefu na najua,” aliongeza beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa.
Mmoja kati ya wachezaji ambao alirudi katika kambi ya City akiwa amezidisha uzito ni kiungo wa kimataifa wa Ufaransa, Samir Nasri, ambaye alipelekwa katika kikosi cha vijana kufanya mazoezi.