Google tag

lundi 14 novembre 2016

AFOTY: Wasifu wa Riyad Mahrez

"Utadhani ameweka gundi katika mguu wake kutokana na vile mpira unavyokwama''. Hayo yalikuwa maoni ya awali ya rafikiye mgombea wa taji la mchezaji bora wa mwaka 2016 barani Afrika Riyad Mahrez, Madjid.

''Tulikuwa tukipigana ili Riyadh ajumuishwe katika kikosi chetu," aliongezea, akikumbuka vile walivyotumia muda wao kucheza soka wakati walipokuwa watoto huko Beni Snous mji uliopo Kaskazini magharibi mwa Algeria.

''Sasa dunia nzima inafahamu uwezo wa Mahrez wa kuucheza mpira anavyotaka na sasa ni klabu kubwa duniani wala sio vijana wenzake wanaotaka ajiunge nao''.
Baada ya kuisaidia Leicester kushinda taji la ligi kuu nchini Uingereza mwaka 2016, katika kile kilichoonekana kuwa kisa cha kushangaza na cha kihistoria, klabu za Arsenal, Barcelona na Chelsea zilitaka kumsajili.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Algeria alikuwa ametangazwa kuwa mchezaji wa kulipwa wa mwaka, akiwa raia wa kwanza wa Afrika kupata taji hilo baada ya kuanzisha kampeni hiyo akicheza wingi ya kulia kwa kufunga mabao 17 kutoa usaidizi wa mabao mara 11 katika mechi 34 za ligi kuu.

Ulikuwa msimu ambapo Mahrez ambaye alijiunga na Leicester kutoka Le Havre kwa pauni 400,000 pekee mwaka 2014, aliimarika na kuisaidia timu yake pamoja na yeye mweyewe kufaidika zaidi ya ndoto yao.

Pengine siku iliyong'arisha nyota ya mchezaji huyo inayopaswa kuwekwa katika kumbukumbu ilikuwa Februari 6 nyumbani kwa mabingwa watetezi wa ligi ya Uingereza Manchester City wakati Mahrez alipougusa mpira na kumpita Nicolas Otamendi, akamchenga Martin Demichelis kabla ya kupiga mkwaju mkali katika lango la Man City ulioiweka Leicester kifua mbele 2-0.

Leicester ilishinda mechi hiyo 3-1 huku Mahrez akisaidia kupata mabao matatu katika mechi nyingine hatua ambayo iliisadia timu hiyo kuwa na ufanisi mkubwa na kushinda ligi.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana hakuwashangaza wengi alipoanza kusakwa na klabu kubwa.

Timu zilianza kuitafuta saini ya mchezaji huyo mwembamba kwa maumbile, mchezaji ambaye umahiri wake umeleta hewa safi katika wingi na kuwafurahisha mashabiki na amekuwa tegemeo la wenzake.

Lakini mchezaji huyo amekataa kujiunga na klabu hizo kubwa na kusema kuwa alitaka kucheza katika klabu hiyo kwa msimu mwengine ili kuthibitisha uwezo wake.
Ameifungia Leicester mabao manne tayari msimu huu matatu kati yao yakitoka katika ligi ya vilabu bingwa ulaya.

Na amekuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha kuwa Algeria inafuzu katika michuano ya kombe la mataifa bingwa Afrika itakayochezwa nchini Gabon.
''Riyad anaifanya timu yake ya taifa kuwa kubwa. Kila mtu anaijua Algeria kutokana na umaarufu wa Riyad." alisema mchezaji mwenza wa Algeria Mehdi Abied.
''Nchini Algeria tunajivunia sana Riyad. Sio rahisi kuwa mchezaji bora wa ligi ya Uingereza. Ni kitu kikubwa sana''.

"Kila mtu barani Afrika anampenda Riyad. Nakumbuka tulienda Ethiopia na Algeria na walikuwa wanamshabikia Riyad zaidi ya wachezaji wa timu yao''!

Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball

Rooney amuahidi jezi kijana anayeugua saratani

Nyota wa timu ya soka ya Uingereza Wayne Rooney ameahidi kumpatia jezi yake mtoto anayeugua kufuatia ushindi dhidi Scotland England.

Kijana huyo amekuwa akifanyiwa kampeni katika mitandao ya kijamii.

Kasabian Newton-Smith mwenye umri wa miaka 8 kutoka Sheffield alipatikana na saratani alipokuwa mchanga na sasa ana uvimbe mara mbili katika kichwa chake.

Klabu za soka,wachezaji na watu binafsi wametakiwa kuchapisha ujumbe wa Twitter #1LastSmile4Kasabian.

Katika ujumbe wa kanda ya video,nahodha huyo wa Uingereza alisema kuwa wachezaji wenzake wanajivunia na ujasiri ulioonyeshwa na Kasabian.