Msichana ambaye alitaka mwili wake ugandishwe na kuhifadhiwa kwa matumaini kwamba anaweza kurejeshewa uhai wakati mmoja siku za usoni, alipata ushindi wa kihistoria saa chache baada ya kufariki dunia.
Msichana huyo alitaka mwili wake uhifadhiwe kwenye friji maalum baada ya kufa kwa matumaini kwamba anaweza kurejeshewa uhai, na hata ikiwezekana aponywe, baadaye. Mamake alimuunga mkono lakini babake alikuwa anapinga wazo hilo.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 14 alikuwa anaugua aina nadra sana ya saratani.
Jaji katika mahakama ya Uingereza aliamuru kuwa mama yake ndiye angekuwa na usemi wa mwisho kuhusu mwili wake.
Mwili wa msichana huyo, aliyefariki mwezi Oktoba, sasa umesafirishwa kwa ndege hadi Marekani kuhifadhiwa.
Msichana huyo alikuwa anaishi London na alitumia mtandao wa intaneti kusoma zaidi kuhusu teknolojia ya kuhifadhi miili ya cryonics miezi ya mwisho ya uhai wake.
Matumaini siku za usoni
Cryonics ni teknolojia inayotumia kuuhifadhi mwili kwa kuugandisha kwa matumaini kwamba huenda ikawezekana kuufufua au kupata tiba siku za usoni.
Msichana huyo alimwandikia jaji na kumwambia kwamba alitaka "kuishi muda mrefu" na hakutana "kuzikwa ardhini".
Aliandika: "Nafikiri kuhifadhiwa kwa teknolojia ya cryonic kutanipatia fursa ya kutibiwa na kuamshwa - hata kama ni baada ya miaka mia moja."
Jaji Justice Peter Jackson, alimtembelea msichana huyo hospitalini na anasema aliguswa sana na ujasiri ambao msichana huyo alikuwa nao katika kukabiliana na maradhi aliyokuwa anaugua.
Kwenye uamuzi wake, alisema, uamuzi huo haukuwa kuhusu usahihi au kutofaa kwa cyronics bali mzozo kati ya wazazi wa msichana huyo kuhusu hatima ya mwili wa binti yao.
Mwili kugandishwa
Cryonic ni shughuli ambayo imekuwa na utata mwingi na hakuna ajuaye iwapo inawezekana kufufua miili iliyogandishwa kufikia sasa.
Kuna vifaa Marekani na Urusi ambapo miili inaweza kuhifadhiwa kwenye madini ya naitorjeni kwenye baridi kali (chini ya nyozijoto -130C) - lakini huduma hiyo haipo Uingereza.
Gharama ya kugandisha mwili kwa muda usiojulikana inakadiriwa kuwa takriban £37,000.
------------------------------------------------------
Barua ya msichana kwa jaji
"Nimetakiwa kueleza ni kwa nini nataka jambo hili lisilo la kawaida lifanyike.
"Nina miaka 14 pekee na sitaki kufariki dunia lakini najua nitafariki dunia.
"Nafikiri kuhifadhiwa kwa njia hii ya cyronic kutanipa fursa ya kutibiwa na kuamshwa - hata kama ni miaka mia moja ijayo.
"Sitaki kuzikwa ardhini.
"Ninataka kuishi na niishi muda mrefu na nafikiri siku za usoni huenda kukapatikana tiba ya saratani ninayougua na kuniamsha.
"Ninataka kupata fursa hii.
"Hayo ndiyo mapenzi yangu.
Wazazi wa msichana huyo walitalakiana na msichana huyo hakuwa amekutana na babake kwa miaka sita kabla yake kuanza kuugua.
Mamake aliunga mkono mapenzi yake ya kutaka mwili wake uhifadhiwe kwa kugandishwa lakini babake alikuwa anapinga.
Babake alisema: "Hata kama itawezekana afufuliwe na atibiwe tuseme miaka 200 ijayo, huenda hatapata jamaa yeyote anayemjua na huenda asikumbuke mambo mengi. Atakuwa katika hali ya masikitiko ikizingatiwa kwamba ana miaka 14 na atakuwa Marekani."
Ingawa baadaye alibadili msimamo wake na kusema anaheshimu uamuzi wa bintiye, alitaka kuuona mwili wa bintiye baada ya kifo chake, jambo ambalo msichana huyo alikuwa amekataa.
Jaji alisema ombi la msichana huyo lilikuwa la kipekee kuwahi kuwasilishwa England na Wales, na labda kwingineko.
Kuhitajika kwa sheria
Jaji Jackson alisema kesi hiyo ni mfano wa matatizo mapya yanayoletwa na sayansi kwa wanasheria.
Msichana huyo alifariki Oktoba akifahamu kwamba mwili wake ungegandishwa, lakini jaji alisema kulikuwa na matatizo siku aliyofariki.
Wahudumu wa hospitali na wakuu wao walieleza wasiwasi kuhusu jinsi mwili wake uliandaliwa kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Hilo lilifanywa na kundi la watu wa kujitolea Uingereza kabla ya mwili huo kupelekwa Marekani.
Amedokeza kwamba mawaziri wanafaa kutafakari uwezekano wa kutoa kanuni na sheria za kusimamia uhifadhi wa miili kwa kutumia teknolojia ya cyronic siku za usoni.