Google tag
mercredi 31 mai 2017
mardi 30 mai 2017
Totti kuaga AS. ROMA
Francesco Totti alitokwa na machozi alipokuwa anaaga baada ya kucheza mechi yake ya mwisho katika klabu ya AS Roma.
Mshambuliaji huyo wa umri wa miaka 40 amechezea klabu hiyo kwa miaka 25.
Katika kipindi hicho, amefunga mabao 307 katika mechi 786 alizocheza.
Aliingia uwanjani mara ya mwisho dakika ya 54 mechi yao dhidi ya Genoa.
Roma walishinda 3-2 kupitia bao la dakika ya mwisho la Diego Perotti ambalo liliwahakikishia nafasi ya kucheza hatua ya makundi Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Baada ya mechi, Totti alisoma barua kwa mashabiki, na kusema: "Naogopa. Sijui siku za usoni zitakuwaje."
"Tafakari, kwamba wewe ni mtoto na umo katikati ya ndoto nzuri...na mamako anakuamsha uende shuleni.
"Unajaribu kurejea kwenye ndoto yako...unajaribu sana lakini huwezi.
"Wakati huu si kwamba ni ndoto, ni uhalisia. Na siwezi kurejea tena."
Nahodha Totti pia alipewa nambari 10 iliyowekwa kwenye fremu, nambari ya jezi yake.
Mkewe na watoto pia walikuwa uwanjani.
Anatarajiwa kuwa mkurugenzi katika klabu ya Roma lakini kumekuwepo na taarifa kwamba huenda akaelekea kwingine.
mercredi 17 mai 2017
Wafungwa wauawa wakijaribu kutoroka jela DRC
Idadi ya wafungwa wasiojulikana wameuawa kwa kupigwa risasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mapema leo baada ya jaribio la kuhepa kutoka gereza kubwa lililoko mjini Kinshasa.
Waziri wa sheria nchini humo, Alexis Thambwe Mwamba amesema baadhi ya wafungwa wapatao 100 wamekamatwa huku wengine hamsini na watano wakiendelea kusakwa.
Miongoni mwa wanaodaiwa kufanikiwa kutoroka ni mfungwa mmoja aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha gerezani kwa mauaji ya rais wa zamani wa DRC, Laurent Kabila.
Maafisa wa usalama wameanzisha oparesheni kali mjini Kinshasa ili kuwakamata wafungwa hao.
Aidha, baadhi ya wafungwa wameuawa kwa kupigwa risasi wakijaribu kukimbia .
Mwandishi wa BBC mjini Kinshasa anasema amewaona maafisa wa shirika la Msalaba Mwekundu, wakikusanya miili yao.
Miili ya waliofariki imepelekwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti mjini Kinshasa.
Hii sio mara ya kwanza kwa wafungwa kutoroka kutoka magereza nchini DRC kwani Januari mwaka uliopita, kisa kama hicho kilishuhudiwa mashariki mwa taifa hilo ambapo wafungwa hamsini walitoroka.
Miongoni mwa waliofanikiwa kutoroka ni wafungwa wa kesi za mauaji na ubakaji.
Mamlaka za magereza zimelaumiwa kwa visa hivyo kwa ulegevu huku magereza mengi yakiwa na msongamano.
Mashirika ya kutetea haki za kibanadam yanalaumu idara ya mahakama kwa kutokamilisha kesi haraka.
Sheddy Clever aiomba serikali kutumbua maprodyuza feki
Mtayarishaji wa muziki nchini, Sheddy Clever ameitaka serikali iweke sheria na viwango vya kudhibiti watayarishaji wa muziki feki ambao ni chanzo cha kusababisha nyimbo kutodumu mda mrefu katika tasnia hali inayopelekea kushuka kwa muziki bongo.
Sheddy amedai serikali inapaswa pia kusimama na kuangalia maslahi ya watayarishaji wa muziki kwani wamekuwa wakiwatajirisha wasanii huku wao wakibaki kwenye maisha yale yale.
“Maprodyuza feki ni wengi sana wale waliopo real ni wachache sana. Zamani kina P -Funk walikuwa wanatengeneza nyimbo zinadumu muda mrefu na ni kali lakini za sasa hivi imebidi ma director wa video wawe wabunifu kutengeneza video kali ili wimbo uonekane ni mzuri,” Sheddy alikiambia kipindi cha Planet Bongo cha EA Radio.
Aongeaza, “Upande wa maslahi inabidi serikali ijipange ituwekee maslahi mazuri kwani mtayarishaji wa muziki kama anahitaji maisha mazuri itambidi awe anakazi nyingine na siyo kutegemea production tuu. Unaweza ukawa na hit kibao redioni lakini maisha yako yakawa ya tabu sana,”
Mtayarishaji huyo ameshatengeneza hit nyingi ikiwemo ‘Marry You’ ya Diamond na Ne-Yo.
Memphis Depay azua gumzo katika tuzo ya mchezaji bora Ufaransa
Mshambuliaji wa klabu ya Lyon, Memphis Depay, amepokea tuzo yake ya bao bora la mwaka. Wakati akienda kupokea tuzo hiyo ya heshima, ameonekana kuvalia Jacket lake mithili ya Msanii nguli wa Pop Duniani, Michael Jackson.
Nyota wa zamani wa Uholanzi Frank de beor aliwahi kumuonya Depay kwa kumtaka aweke akili yake zaidi uwanjani kabla ya kujiingiza katika mambo mengine ya nje ya uwanja.
mardi 9 mai 2017
Jaji wa mahakama kuu afungwa jela India
Mahakama ya juu zaidi nchini ndia imemhukumu jaji wa mahakama kuu ya Calcutta, kifungo cha miezi sita gerezani.
Jaji Chinnaswamy Swaminathan Karnan ndiye jaji wa kwanza wa mahakama kuu kufungwa gerezani katika historia ya nchi hiyo.
Jaji Karnan, amepatikana na kosa la kudharau mahakama siku moja baada ya hatua yake ya kujaribu kumhukumu jaji mkuu wa India na majaji wengine sita wa mahakama ya juu zaidi kifungo cha miaka mitano Jela.
Katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwepo na hali ya mvutano na majibizano katika mahakama ya juu nchini India.
Mwezi Januari Jaji Chinnaswamy Karnan aliwashutumu majaji kadhaa wa mahakama ya juu nchini India kwa kuwa wafisadi.
Katika shutma hizo jaji huyo wa mahakama ya juu alimwandikia waziri Mkuu waraka maalum akitaka kuungwa mkono kwa juhudi zake zake za kutaka majaji hao wa mahakama wakamatwe, wachunguzwe na kutupwa jela miaka tano kwa madai ya ufisadi.
Kwanzia wakati huo uhasama kati yake na majaji wa mahakama ya juu nchini India ukazidi.
Majaji hao wakamtumia ilani wakimtaka afike mbele yao kwa kujibu mashataka ya kuwaharibia majina.
Hata hivyo alipuuza agizo hilo.
Jaji mkuu wa nchi hiyo katika siku za hivi karibuni ametoa agizo kwamba jaji huyo apelekwe hospitali kupimwa akili kwani alisema wanadhani kwamba si mzima wa akili.
Mwanafunzi anayefanana na Lionel Messi nchini Iran azua gumzo
Mwanafunzi mmoja nchini Iran amelazimika kupelekwa katika kituo cha polisi mwishoni mwa wiki iliyopita kisa na mkasa! Kufanana kulikokithiri na Lionel Messi.
Watu wengi katika mji wa Hamaden wamekuwa wakiomba kupiga picha na kijana huyo aitwaye Reza Parastesh, na hivyo kusababisha msongamano wa watu kila atakakokanyaga, hivyo polisi walilazimika kumhifadhi kwa muda ili kuondoa msongamano huo.
Mchanganyiko huo ulianza miezi michache iliyopita wakati baba wa kijana huyo aliyefanana mno na Messi alipompiga picha akiwa amevalia fulana ya timu ya Barcelona yenye namba kumi.
Reza Parastesh, ana umri wa miaka ishirini na mitano kwa sasa, hivi karibuni alianzisha mtindo wa ukataji nywele na kupunguza ndevu zake mithili ya mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Argentina .
Reza Parastesh, kwa sasa amebatizwa jina 'Messi wa Iran' amejikuta kila wakati na kila mahali akiombwa kupiga picha na watu wa aina kwa aina katika mji wa nyumbani kwao Hameden, nchini Iran.
Kijana huyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kwa sasa watu wananiona mimi kuwa ndiye Messi wa Iran na kunitaka nifanye kiila kitu afanyacho Messi halisi, na pindi ninapotokeza mahali, watu hupatwa na mshtuko.
Nina furaha kubwa kuona kwamba ninawapa furaha na hili linapotokea linanipa ari mpya.
Parastesh aka Messi amekuwa ni mtu mwenye kufanyiwa mahojiano ya mara kwa mara na vituo vya habari na kufanikiwa kusaini mikataba mikubwa ya uoneshaji mavazi, na sasa ana fanya mazoezi makubwa ya kujua mbinu za mpira wa miguu ili akidhi vigezo vya Messi halisi.
samedi 6 mai 2017
Picha za utupu za mgombea urais Rwanda zavuja mtandaoni
Baada ya siku chache za Diane Shima Rwigara kutoka Rwanda kutangaza kugombea urais nchini humo, hatimaye amekutwa na skendo ya kuvujisha picha zake za utupu mtandaoni.
Diane 35, ambae ni msomi wa Uchumi na mtoto wa aliyekuwa tajiri maarufu nchini Rwanda Asinapol Rwigara, picha zake za utupu zilianza kusambaa mapema jana nchini Rwanda hususani kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp na Facebook na baadae kutapakaa duniani kote.
Kwa mujibu wa mtandao wa Habari Pevu umeeleza kuwa picha hizo zilitumwa awali kwa njia ya e-mail na mtu aliyejiita ni Muandishi wa habari aliyejulikana kwa jina la Twahirwa Emmy huku akishinikiza kuwa mrembo huyo hafai kuchaguliwa kuwa Rais kwa vitendo vyake vichafu vya kupiga picha za utupu.
Hata hivyo Jitihada za kumpata mrembo huyo kuzungumzia picha hizo zilizovuja ziligonga mwamba baada ya waandishi wa habari nchini Rwanda kumsaka bila mafanikio.
Uchaguzi mkuu wa Rais nchini Rwanda unatarajiwa kufanyika mwaka huu mwezi wa Augosti, na mpaka sasa kuna wagombea watatu tuu ambao ni Mpayimana Philippe ambae ni mgombea binafsi na Franck Habineza kutoka chama cha Green pamoja na Diane Rwagira wote wakitarajiwa kuleta upinzani mzito kwa Rais Paul Kagame .
jeudi 4 mai 2017
Aaron Lennon kuugua ugonjwa wa ki Akili
Winga wa klabu ya Everton Aaron Lennon amezuiliwa chini ya kifungu cha polisi cha afya ya kiakili kuhusu wasiwasi wa hali yake.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alipelekewa hospitalini kwa ukaguzi wa kiafya baada ya maafisa wa polisi kuitwa katika eneo la Salford siku ya Jumapili.
Lennon kwa sasa anapata matibabu kwa ugonjwa unaosababishwa na shinikizo la kiakili ,kulingana na klabu hiyo.
Mchezaji huyo wa Uingereza aliyejiunga na Everton kutoka Tottenham 2015 hajachezea kikosi cha kwanza tangu mwezi Januari.
Maafisa wa polisi wa Manchester walisema: Polisi waliitwa saa kumi na nusu mchana kufuatia wasiwasi wa mtu mmoja aliyekuwa katika barabara ya zamani ya eneo la Eccles .
Maafisa wa polisi waliitikia wito huo na mtu mwenye umri wa miaka 30 alikamatwa chini ya kifungu cha 136 cha afya ya kiakili na kupelekwa hositali kwa ukaguzi.
Habari kuhusu kulazwa kwa Lennon zilivutia ujumbe wa kumuombea katika mitandao ya kijamii miongoni mwa wachezaji wa soka na mashabiki wa klabu yake ya zamani na ya sasa.
Conte: Kuna Antonio wawili, na mmoja ni mnyama
Meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte amesema yeye huwa "mnyama" wakati wa mechi, baada yake kushuhudia viongozi hao wa Ligi ya England wakilaza Everton 3-0 Jumapili.
Mwitaliano huyo alisherehekea uwanjani na wachezaji wake baada ya mchezo kumalizika Goodison Park, ambapo mabao yalifungwa na Pedro, Gary Cahill na Willian.
Chelsea wanahitaji kushinda mechi tatu kati ya nne walizosalia nazo msimu huu kushinda taji la ligi, msimu wa kwanza chini ya Conte.
"Kuna Antonio wawili. Ni watu wawili tofauti," alisema Conte, 47.
"Wakati wa mechi, najua kwamba mimi huwa mnyama.
"Baada ya mechi, lazima niwe nimetulia baada yetu kushinda lakini nafikiri ni vyema kusherehekea (ushindi) na wachezaji, wafanyakazi na mashabiki. Hili lina maana kubwa katika maisha yangu."
Conte, ambaye alishinda mataji matatu mtawalia ya ligi ya Serie A akiwa na Juventus kati ya 2012 na 2014, anafahamika sana kwa vituko vyake na nguvu anazoonekana kuwa nazo akielekeza mechi inapokuwa inaendelea.
Alisherehekea mabao ya klabu yake dhidi ya Everton kwa kuruka na kurusha ngumi hewani na kukimbia sehemu inayotengewa wakufunzi nje ya uwanja.
Mwitaliano huyo huwa ametulia wakati wa mahojiano na wanahabari kabla na baada ya mechi, sifa ambazo anasema huwa anapenda wachezaji wake wawe nazo.
"Lazima tuwe na furaha kwa sababu tulicheza mchezo kwa kutumia vichwa vyetu, na kipindi kama hiki katika msimu, ni muhimu kutumia vichwa vyetu, kisha moyo na baadaye miguu," alisema.
Conte anaamini sana kuhusu hilo, kiasi kwamba aliandika kitabu chenye kichwa Testa, cuore e gambe (Kichwa, moyo na miguu) mwaka 2014.
Mechi za Chelsea zilizosalia 2016-17
#Jumatatu, 8 Mei Middlesbrough (Nyumbani)
#Ijumaa, 12 Mei West Brom (Ugenini)
#Jumatatu, 15 Mei Watford (Nyumbani)
#Jumapili, 21 Mei Sunderland (Nyumbani)
#Jumamosi, 27 Mei Arsenal (fainali Kombe la FA)
lundi 1 mai 2017
Sulley Muntari apewa kadi ya manjano akilalamikia kubaguliwa
Mchezaji wa Pescara Sulley Muntari, aliondoa uwanjani baada ya refa kumpa kadi ya manjano, alipolalamika kuwa alikuwa akidhulumiwa kwa misingi ya rangi wakati wa mechi.
Kiungo huyo wa zamani wa Ghana mwenye umri wa miaka 32, alimuomba refa Daniele Minelli asimamishe mechi hiyo ya Jumapili.
Lakini badala yake refa alimpa kadi ya manjano dakika ya 89, hatua iliyosababisha mchezaji huyo wa zamani ya vilabu vya Portsmouth na Sunderland kupinga kwa kuondoka uwanjani.
Kwa hasira aliwakabili mashabiki wa klabu ya Cagliari akisema kwa sauti. "Hii ni rangu yangu."
Akiongea baada ya mechi Muntari alisema: "Refa hastahili kukaa tu uwanjani na kupiga firimbi, ni lazima afanye kila kitu.
"Ni lazima aone vitu hivi na kuonyesha mfano.
"Nilimuuliza ikiwa alikuwa amesikia matusi. Nikasisitiza kuwa ni lazima asimamishe mechi."
Meneja wa Pescarfa Zdenek Zeman ambaye upande wake ulishindwa kwa bao 1-0, alisema kuwa alimuomba refa kuingilia kati lakini akasema hakuona wala kusikia chochote.