Dada mmoja akiwa ofisini alipigiwa simu kuwa mwanae amepata ajali wakati anatoka shule, alikuwa ameumia sana. Kwa harakaharaka yule dada aliwasha gari na kuanza safari kuelekea hospitali ili kumuona mwanae.
Akiwa njiani katika mistari ya Zebra huku akiwa na mawazo alitaka kumgonga Kaka mmoja ambaye alikuwa akivuka barabara kwa kukimbia. Katika kumkwepa gari iligonga ukingo wa barabara na kukwaruizika kidogo.
Kwa hasira yule dada alishuka na kuanza kumtukana yule kijana kuwa kamsababishia ajali na kumchelewesha. Alimtukana sana, hali iliyowafanya watu kujaa. Watu walipofika walianza kuuliza nini ndipo yule dada kwa uoga alidanganya kuwa yule kaka alitaka kumuibia.
Watu walianza kumpiga Kaka wa watu kama mwizi, kuona vile yule dada aliingia kwenye gari na kuelekea hospitalini kumuona mwanae. Huku nyuma Polisi walikuja na kumuokoa yule kijana lakini akiwa ameumizwa sana.
Alifika hospitalini na kumkuta binti yake akiwa katika hali mbaya, alikuwa akitakiwa kufanyiwa upasuaji wa haraka ili kuokoa maisha yake, manesi walishamuandaa mtoto na alikuwa akisubiriwa Daktari ambaye alipigiwa simu na alikuwa njiani.
Wakati wakimsubiri Daktari, Nesi alikuja na kuwamabia kuwa, wampeleke hospitali nyingine kwani Daktari waliyekuwa wakimsubiri asingeweza kumfanyia upasuaji mtoto wao kwani alikuwa amepigwa na wananchi wakati akija hospitalini wakimuita mwizi.
Dada na mumewe walichanganyikiwa, mtoto kutokana na hali yake mbaya alichukuliwa harakaharaka na gari la wagonjwa ili kuhamishwiwa hospitalini nyingine. Wakati wanatoka kuelekea kwenye gari kulikuwa na gari ya Polisi inaingia.
Kijana mmoja akiwa hoi alishushwa, yule Dada alimtambua ni yule kijana ambaye alimuitia mwizi kule barabarani. Kwa hasira yule Dada allimuambia Mume wake.
“Huyu Kaka namfahamu ni kibaka tu alitaka kuniibia, ndiyo amenichelewesha kufika huku hospitalini!”
Nesi ambaye alikuwa akimsaidia kumpandisha mtoto katika gari la wagonjwa alimkatisha na kusema.
“Hapana Dada huyu kaka si kibaka, ni Daktari ambaye alipaswa kumfanyia upasuaji mwanao. Amepigwa wakati akikimbia kuja hospitalini, mimi ndiyo nimempigia simu kuja…”
Dada wawatu nguvu zilimuishia ilibidi anyamaze, walifika hospitali nyingine, mtoto alikuwa katika hali mbaya. Aliandaliwa na kuingizwa katika chumba cha upasuaji lakini kabla hajafanyiwa chochote yule mtoto alifariki.
Baada ya uchunguzi ilionekana damu ilishaingia kwenye ubongo. Wangeweza kuokoa maisha yake kama angefanyiwa upasuaji katika hospitali ya mwanzo, kule kusafirishwa tena na kurushwa rushwa barabarani kulisababisha damu kuendelea kuvuja kwa kasi ndani.
Yule dada alizimia baada ya kupata habari zile, maneno yake yalisababisha kuondoa maisha ya mwanae.
FUNZO
Usimdharau mtu kutokana na hali yake kwani hujui ni kitu gani anaweza kukusaidia.