Cristiano Ronaldo alifunga mabao matatu na kuwawezesha mabingwa watetezi wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Real Madrid kuwatimua Bayern Munich kutoka kwenye michuano ya msimu huu katika hatua ya robofainali.
Mechi hiyo iliyomalizika 4-2 hata hivyo ilijaa utata na mshindi alipatikana katika muda wa ziada.
Kiungo wa kati wa Bayern Munich Arturo Vidal alitimuliwa uwanjani dakika ya 84 jambo ambalo lilionekana kuathiri mwelekeo wa mechi hiyo.
Ronaldo naye alionekana kuwa alikuwa ameotea alipokuwa anafunga bao la pili la Real muda wa ziada.
Bayern, ambao walihitaji mabao mawili kusonga, alikuwa wameongoza kupitia penalti iliyofungwa na Robert Lewandowski.
Madrid walitatizika kutamba kwenye mechi hiyo iliyochezewa Bernabeu kabla ya Ronaldo kufunga kwa kichwa kutokana na krosi ya Casemiro.
Bayern walijibu sekunde 36 baadaye Sergio Ramos alipojifunga na kulazimisha mechi hiyo kuingia muda wa ziada.
Ni hapo ambapo Ronaldo alifunga bao la utata la Madrid.
Nahodha huyo wa Ureno kisha alifunga la tatu - lake la 100 katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya. Marco Asensio aliwakamilishia ushindi kwa kuongeza la tatu.
Madrid watamfahamu mpinzani wao nusufainali wakati wa droo Ijumaa.
Majirani wao Madrid Atletico Madrid walisonga kwa kuwaondoa Leicester City.
Kwenye robofainali hizo nyingine, Barcelona wanakutana na Juventus nao Monaco wakutane na Borussia Dortmund baadaye Jumatano.