Rais wa Liberia George Weah amelifahamisha baraza la seneti kuwa anapanga kukaa siku tisa nchini Qatar kutazama mechi za kombe la dunia .
Bw Weah - mwanasoka wa zamani - aliondoka nchini wiki iliyopita kwa ziara kadhaa za kigeni, lakini sio mipango yake yote imefichuliwa.
Mwanawe Timothy, ambaye ni Mmarekani, atakuwa katika kikosi cha Marekani katika mashindano ya Kombe la Dunia, yatakayong'oa nanga tarehe 20 Novemba.
George Weah alichezea timu kubwa za Ulaya, zikiwemo AC Milan na Chelsea.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 56 alibadili kazi na kuchaguliwa kuwa rais wa Liberia mwaka wa 2017.
Habari za mipango ya safari ya nje ya rais zimewakasirisha raia wengi wa Liberia, wengine wametumia vipindi vya kupiga simu kwenye redio na kwenye mitandao ya kijamii kumkosoa.
Wanasema itakuwa ni kutotilia maanani hali ya wananchi kwa rais kwenda Qatar wakati ambapo watu wengi walikuwa wakikabiliana na tatizo kubwa la chakula, pamoja na kutokuwa na uhakika kuhusu mwenendo wa sensa ya watu iliyocheleweshwa sana, ambayo Bw Weah aliiahirisha hivi majuzi kwa mara ya sita.
Wafanyakazi wa Bw Weah - ambao hawajajibu maswali kuhusu gharama ya safari hiyo - wamejibu wakosoaji wake, wakisema ziara za nje za rais "zitazaa faida kubwa" kwa nchi.