Dah nimechanganyikiwa kabisaaa. Akili
haifanyi kazi, yaani dah hata sijui nianzie wapi. Picha imekuwa
chengachenga kabisa. Unajua kiukweli, nilikuwa nimepanga kuwa nianze
wiki hii mipango ya harusi yangu, nilikuwa nataka harusi iwe mwezi wa
sita mwaka kesho, nilishatayarisha bonge ya plani, nilikuwa nimeipanga
kisayansi kabisa. Sasa mambo yanaharibika mbele yangu na sina la
kufanya, nimechanganyikiwa.
Kuna mtoto mmoja wa kike mtaani kwetu,
wengi mnamfahamu maana anaonekana kwenye runinga karibu kila wiki na
kwenye magazeti ndiyo hakosi, mtoto anawaka, guu guu, sauti kama
kinanda, shepu ya katalogi. Sasa huyo ndiye niliyepanga kumuoa,
nilipanga harusi iwe ya kiwango cha kimataifa, yaani jambo hili
lingetikisa vyombo vya habari kwa muda mrefu.
Hata baada ya harusi vyombo vya habari
vingetufuatilia sana, mtoto wetu naye angekuwa maarufu, tungemtumia
kwenye matangazo na kukusanya mkwanja wa kueleweka, picha nilikuwa
nimeipanga kwa kuangalia mipango ya muda mfupi na muda mrefu. Yaani kila
kitu nilikwishakipanga vizuri sana sasa dahh picha inaungua taratibu.
Yaani ilipotangazwa tu kuwa mjomba wangu
kashinda Ubunge, nikajua sasa maisha yangu yanabadilika, nilianza
kuimba ule wimbo wa Vijana Jazz Band unaitwa Umaskini Bye Bye. Mimi na
mjomba tuko karibu sana tangu nikiwa mdogo, mjomba wangu alikuwa
akinipenda sana.
Niliona wazi kabisa kuwa mjomba wangu
atachaguliwa kuwa waziri, tena ikawezekana hata kuwa waziri mkuu. Sasa
kasheshe lilianza baada ya kuona kwanza mjomba amekwisha ukosa uwaziri
mkuu, na sasa nimemsikia rais kafuta safari za nje za mawaziri kabla
hata hajawataja, yaani ndoto ndiyo imeharibika kabisaaa.
Unajua huyu mtoto kwa kweli sijaongea
naye, nilikuwa nangoja mjomba akichaguliwa kuwa waziri ndiyo nimuibukie
na kumhakikishia kuwa maisha ya kifahari akikubali tu kuolewa na mimi.
Harusi yetu yetu ingekuwa Uswisi, hanimuni Australia, na kote huko
mjomba angekuwa mgeni rasmi, sasa mkuu wa nchi katangaza hakuna safari
za nje, tena kaanza hata kupunguza gharama za sherehe, ni wazi ndoto
yangu haitatimia hata mjomba akipata zari la kuwa waziri. Ndiyo mjue
sioi tena hivyo, dahh, kweli Hapa Kazi Tu!
Aucun commentaire:
Enregistrer un commentaire