Alibaba

jeudi 3 novembre 2016

Kichapo chaibua hasira za Messi

HAKUNA mwanadamu anayekubali kushindwa kirahisi. Lionel Messi anaonekana mpole kumbe nyuma ya upole huo kuna mambo, unaambiwa jamaa ni ngumi mkononi. Imetokea juzi baada ya Barcelona kuchapwa mabao 3-1 katika dimba la Etihad jijini Manchester.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Hispania, inadaiwa kuwa Messi alitiana mkononi na mchezaji mmoja wa Manchester City wakati akielekea katika vyumba vya kubadilishia nguo mara baada ya kumalizika kwa pambano la juzi.
Ripoti zinadai kwamba mchezaji huyo wa Manchester City alimwambia kitu nyota huyo wa kimataifa wa Argentina lakini kikamkera kiasi cha kumuita mchezaji huyo wa City kuwa Mpumbavu na hapo ndipo walipotiana mkononi.

Kwa mujibu wa habari za ndani kutoka Hispania, Messi ambaye anasifika kwa upole na nidhamu alikasirika kiasi cha kwenda katika chumba cha kubadilishia nguo cha Manchester City kwa ajili ya kugombana na staa huyo wa City.

Hata hivyo, rafiki mkubwa wa Messi nyota mwenzake wa kimataifa wa Argentina, Sergio Aguero wa Man City ambaye katika pambano hilo alipika bao moja la Man City ndiye aliyegeuka kuwa msuluhishi wa ugomvi huo ambao uliwashangaza wengi.

Messi alifunga bao la kwanza katika pambano hilo lakini kikosi cha kocha, Luis Enrique kilichemsha katika pambano hilo huku kocha wa City, Pep Guardiola ambaye ni kocha wa zamani wa Barcelona akilipiza kisasi cha pambano la kwanza ambalo City ilichapwa 3-1 jijini Barcelona.

Kiungo wa kimataifa wa Ujerumani, Ilkay Gundogan ambaye alinunuliwa kwa dau la Pauni 20 milioni kutoka Borussia Dortmund katika dirisha kubwa la majira ya joto alifunga mabao mawili katika pambano hilo huku staa wa kimataifa wa Ubelgiji, Kevin De Bruyne akifunga bao moja murua la faulo.

Baada ya pambano hilo, Guardiola alionekana kukoshwa na kiwango cha timu yake ingawa alikiri kwamba alikuwa hana furaha sana kwa sababu alikuwa ameifunga timu yake ya zamani Barcelona ambayo ametwaa nayo mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

“Wakati klabu kama Manchester City inapokuwa na miaka 25 bila ya michuano ya Ulaya inakuwa historia. Historia ina maana unapocheza na timu kubwa unakuwa haujiamini kupigana uso kwa uso. Hatukucheza dhidi ya Barcelona, tulicheza dhidi ya utamaduni wetu,” alisema Guardiola ambaye pia aliwahi kuwa staa mkubwa wa
Barcelona.

“Nina furaha. Ni kawaida kwamba haya mambo yanatokea. Nina furaha kwa sababu tumepata pointi tatu. Nimejifunza kwamba wachezaji wangu wanaweza kufanya mashambulizi ya kushtukiza. Lakini kwa upande mwingine nina huzuni kidogo kwa sababu nimeifunga klabu ambayo naipenda sana,” aliongeza Guardiola.

Guardioala pia alimsifu mshambuliaji wake, Sergio Aguero ambaye alianza katika pambano la juzi baada ya kuachwa nje katika pambano la kwanza baina ya timu hizo dimba la Nou Camp wiki mbili zilizopita.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire