Meneja wa Chelsea Antonio Conte amepuuzilia mbali pendekezo kwamba huenda viongozi hao wa Ligi Kuu ya Uingereza wakapokonywa alama kutokana na utovu wa nidhamu.
Chelsea na Manchester City wameshtakiwa kwa kukosa kuwadhibiti wachezaji wao wakati wa mechi kati ya klabu hizo mbili tarehe 3 Desemba.
Baada ya visa kadha awali, bodi ya rufaa ya Chama cha Soka England ilikuwa imeonya Chelsea mnamo Julai kwamba karibu utafika wakati ambapo "adhabu pekee itakayotosha ni kupokonywa alama".
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa hilo kutokea, Conte aliwaambia wanahabari: "Unafanya mzaha? Unatania?"
Chelsea wametozwa faini mara tano na FA kwa kukosa kuwadhibiti wachezai tangu Februari 2015.
Viongozi hao wa EPL awali walitozwa faini ya juu sana ya £375,000 kutokana na mashtaka matatu kutoka kwa mechi ambayo iliisha sare 2-2 wakicheza dhidi ya Tottenham uwanjani Stamford Bridge Mei.
Bodi ya rufaa ilipunguza faini hiyo hadi £290,000 lakini ikashutumu Chelsea kwa kuwa na rekodi mbaya ya kushindwa kuwadhibiti wachezaji.
Mara ya mwisho klabu kupokonywa alama kwa sababu ya utovu wa nidhamu ilikuwa Manchester United na Arsenal waliopokonywa alama kutokana na vurugu zilizotokea Old Trafford Oktoba 1990.
Wakati wa kuadhibu Chelsea kuhusu matukio ya Stamford mwezi Mei, tume ya FA ilisema ilitafakari uwezekano wa kupokonya alama Chelsea lakini wazo hilo likaondolewa kutokana na sababu kwamba Chelsea hawakuwa wamepewa onyo la mwisho.
Chelsea na Spurs walionywa kuhusu mienendo yao siku za usoni lakini FA haikugusia kamwe "onyo la mwisho".
Aucun commentaire:
Enregistrer un commentaire