Rais Barack Obama anapojiandaa kustaafu nchini Marekani wiki ijayo, kuna vitu vya kawaida kama vile maktaba, barabara na shule ambavyo vimepewa jina lake kama heshima kwake.
Kutakuwa na Maktaba ya Rais Barack Obama mjini Chicago. Aidha, kuna shule nyingi zilizopewa jina la kiongozi huyo wa kwanza Mwamerika Mweusi nchini humo.
Lakini kando na hayo, kuna vitu vingi ambavyo huwezi kutarajia vilivyopewa jina lake vikiwemo vimelea na buibui.
Kimelea
Mnyoo ambao kwa kisayansi hufahamika kama Baracktrema obamai ndio kimelea cha pili kupewa jina la Obama.
Mnyoo huu ambao ni mrefu na unafanana na uzi huambukiza kasa wa maji yasiyo na chumi Malaysia na unaweza kuua.
"Hili ni jambo bila shaka, ingawa ndogo tu, ambalo tumefanya kwa heshima ya rais wetu," anasema Dkt Thomas R Platt, mtaalamu wa vimelea wa kasa ambaye aligundua aina hiyo ya mnyoo.
Anasema ni jamaa wa Bw Obama, kwa mbali.
Watafiti wamewahi kuupa mnyoo unaopatikana nchini Kenya jina
Paragordius obamai. Mnyoo huo uligunduliwa karibu na nyumbani kwa rais wa Obama.
Samaki
Kama sehemu ya kutoa heshima kwa Bw Obama kwa juhudi zake za uhifadhi wa viumbe wa baharini katika bahari ya Pasifiki, wanasayansi walimpa samaki mmoja anayepatikana eneo la Kure Atoll katika hifadhi ya Papahānaumokuākea, pwani ya Hawaii jina la rais huyo. Samaki huyo ana rangi ya damu ya mzee na rangi ya dhahabu.
Mwaka 2012, watafiti walimpa jina Etheostoma Obama samaki mwingine wa rangi ya samawati na manjano. Samaki huyo hupatikana katika mito ya Duck na Buffalo inayotoa maji yake kutoka kwa mto Tennessee.
Mjusi
Mjusi wa urefu wa futi moja na aliyekuwa na meno yaliyosimama wima alipewa jina Obamadon, kutokana na tabasamu la Rais Obama. Mjusi huyo aliangamia.
Mlima
Bw Obama ni miongoni mwa marais wa Marekani ambao wana milima iliyopewa majina yao. Taifa la Antigua lilibadili jina la mlima mrefu zaidi nchini humo, mlima wa Boggy kuwa Mlima Obama siku yake ya kuzaliwa mwaka 2009.
Kuvu
Mwaka 2007, watafiti walizipa kuvu (ukungu wa miti na miamba) jina
Caloplaca obamae, Bw Obama alipoanza kufanya kampeni yake ya urais. Walichukua hatua hiyo kwa sababu ya Bw Obama kuunga mkono masomo ya sayansi.
Kituo cha mafuta
Kijiji cha Moneygall katika eneo la Offaly, katikati mwa Dublin na Limerick nchini Ireland, kuna kituo cha mafuta ambacho kilipewa jina la rais huyo wa Marekani.
Katika Barack Obama Plaza kuna kituo cha mafuta, mgahawa na kituo cha wageni ambacho hutoa habari kuhusu uhusiano wa Bw Obama na Moneygall.
Kijiji cha Moneygall ndicho asili ya babake babu wa babu wa Rais Barack Obama
Mkate
Kabla ya Rais Obama kuzuru Ireland, waokaji wa mikate walikimbia kuoka mikate maalum.
Mkazi wa Moneygall Joseph Kearney aliwasilisha mikate maalum kwa watu wa jamaa za Bw Obama nchini Ireland waliokuwa wakijiandaa kwa ziara ya O'Bama.
Ndege
Kuna ndege anayepatikana Amazon magharibi ambaye amepewa jina Nystalus obamai.
Shule Kenya
Katika kijiji cha Kogelo, alikozaliwa babake Obama, kuna shule mbili, Senator Obama Kogelo Primary School na Senator Obama Kogelo Secondary School.
Zilipewa majina hayo Obama alipokuwa seneta wa Illinois.
Buibui
Kuna buibui kwa jina, Aptostichus barackobamaiwa aina ya trapdoor, ambao wamepewa jina hilo kutokana na Rais Obama, ambaye ni shabiki waSpider-Man.
Aina hao wa buibui hupatikana California, na ni miongoni mwa buibui 40 wa familia ya Aptostichus.
Wengine huitwa Aptostichus stephencolberti (kutokana na mchekeshaji Stephen Colbert) na
Aptostichus angelinajolieae (kutokana na mwigizaji Angelina Jolie).
Aucun commentaire:
Enregistrer un commentaire