STAA wa muziki wa Bongofleva na bosi wa lebo ya Next Level Music, Raymond Shaban Mwakyusa (Rayvanny) amefikisha (streams) milioni 100 kupitia jukwaa namba moja la muziki barani Afrika, Boomplay.
Rayvanny ambaye pia ni memba wa lebo kubwa barani Africa, WCB Wasafi, amekuwa msanii wa kwanza nchini kufikisha streams milioni 100 kupitia Jukwaa hilo.
Kwa hatua hii muhimu, Rayvanny anajiunga na wasanii wengine kama vile Burna Boy, Olamide na Fireboy DML miongoni mwa wengine kwenye Golden club ya Boomplay.
Kupitia jukwaa la Boomplay, Rayvanny ndiye msanii wa Kitanzania anayefuatiliwa zaidi akiwa na jumla ya wafuasi zaidi ya laki na nusu huku EP yake ya Flowers II ikiwa EP ndio kazi yake iliyosikilizwa Boomplay ikiwa na zaidi ya streams milioni 30.
Albamu yake ya mwaka 2021 iliyopewa jina la Sound from Africa yenye zaidi ya wasikilizaji milioni 22.9 ni albamu ya nne ya Tanzania ambayo imesikilizwa zaidi baada ya ‘Definition of Love’ ya Mbosso, Album ya Alikiba ya ‘Only One King’, na Albamu ya Harmonize inayofahamika kama ‘High School’.
Meneja Mkuu wa Boomplay nchini Tanzania, Natasha Stambuli amesema, “Rayvanny ni msanii mwenye kipaji kikubwa na kwake kuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki kufikisha streams zaidi ya milioni 100 kwenye jukwaa letu ni jambo ambalo tunajivunia sana.
"Boomplay inaendelea kujiimarisha katika kuhakikisha wasanii wa Afrika wanafikia uwezo wao. Tumefurahi kwa kitu ambacho Rayvanny ameweza kukifanya na kuiwakilisha Tanzania vyema na ni matumaini yangu kwamba hii itawatia moyo wasanii wengine kufanya vivyo hivyo,"amesema na kumalizia Meneja Mkuu huyo.