Google tag

mercredi 14 septembre 2016

Marufuku kubadilishana jezi Man United

Mastaa wakali wa timu hiyo, kuanzia kwa Zlatan Ibrahimovic, Wayne Rooney, Paul Pogba, Juan Mata na wengineo wamepigwa marufuku kubadilishana jezi na wachezaji wa timu pinzani kwa ajili ya kuokoa pesa.
Zlatan analipwa pauni 260,000 kwa wiki, akiwa daraja la juu la malipo kama ilivyo kwa akina Rooney, lakini wameambiwa wasibadilishane jezi zao ambazo kwa kawaida zinagharimu pauni 80 tu kwa kile kinachoitwa kubana matumizi.
Kila mchezaji mmoja wa United anapewa jezi nne kwa ajili ya mwanzo wa msimu ambapo, mbili zinakuwa za mikono mirefu na mbili zinakuwa za mikono mifupi huku pia akipewa bukta nne pamoja na soksi pea nne kuendana na jezi za juu.
Hata hivyo, wachezaji hao uzimaliza jezi hizo mapema kwa kubadilishana na wachezaji wa timu nyingine, lakini pia wamekuwa wakiwapa mashabiki kwa kuwakabidhi mikononi mara baada ya kumalizika kwa mechi mbalimbali.
“Wameombwa wasibadilishane jezi kwa sababu hawatapewa nyingine. Inashangaza sana ukiangalia thamani ya klabu jinsi ilivyo,” alisema mtu mmoja wa ndani wa Manchester United kufuatia agizo hilo.
Licha ya utajiri wa United, agizo hilo linaonekana kufuata nyayo za klabu ya Cambridge United ya madaraja ya chini ambayo mwaka jana katika pambano la FA dhidi ya Manchester United iliwaagiza wachezaji wake wasibadilishane jezi na wachezaji wa United kutokana na ukata uliokuwa unawakabili.
“Wamiliki wana sifa ya kuchunga sana gharama ambazo hazina umuhimu,” aliendelea kusema mtoa taarifa huyo. Hesabu zinaonyesha kuwa kila mchezaji wa United akiamua kubadilishana jezi na mchezaji wa timu pinzani, United itagharamika kiasi cha pauni 660.
Agizo hilo litapokelewa kwa mshangao mkubwa na mashabiki wengi wa soka duniani kote ukizingatia kuwa United ni moja kati ya klabu tajiri duniani ambao msimu huu ilithibitisha utajiri wake kwa kulipwa dau la pauni 89 milioni kwa kumchukua kiungo, Paul Pogba kutoka Juventus huku dau hilo likiwa rekodi ya uhamisho duniani.
Mpaka sasa United inakadiriwa kuwa na thamani ya pauni 3 bilioni ikiwa inafukuzana kwa karibu zaidi na Real Madrid katika nafasi ya juu ya kuwa klabu yenye thamani zaidi duniani na nguvu hiyo imekuwa ikiongezeka kila kukicha.
Julai 2014, ilisaini mkataba wa miaka 10 na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas ambapo thamani ya mkataba huo ni pauni 750 milioni kwa miaka hiyo wakiing’oa kampuni shindani ya Nike. Dau hilo ni sawa na pauni 75 milioni kwa mwaka.
Kwa wakati huo dili hilo lilikuwa kubwa zaidi katika udhamini duniani, lakini sasa limepitwa na dili la kampuni hiyo hiyo kwa klabu pinzani tajiri ya Real Madrid ambayo imeingia mkataba wa pauni 117. 2 milioni kwa kila mwaka.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire