Siku hizi ni vigumu sana kutafakari hali ilivyokuwa kabla ya mafanikio makubwa kupatikana katika teknolojia ya mawasiliano.
Imekuwa kama ada kwamba kila wakati lazima kuwe na habari.
Lakini zamani, hali ilikuwa tofauti kabisa.
Miaka 87 iliyopita, mnamo 18 Aprili 1930, msomaji wa habari katika BBC alikosa cha kutangaza.
Taarifa aliyoisoma wakati wa taarifa ya habari ya saa tatu kasorobo usiku ilikuwa: "Hakuna habari".
Baadaye, kinanda kilichezwa kwa dakika 15 zilizosalia ambazo zilikuwa zimetengewa habari.
Baadaye, matangazo yalipelekwa Ukumbi wa Malkia katika jumba la Langham Place, London ambapo kulikuwa na tamasha la muziki wa Wagner.
Miaka 87 baadaye, hali ni tofauti kabisa. Jumanne ilikuwa siku iliyojaa habari tele.
Watu walipokuwa wanashiriki pilkapilka za hapa na pale baada ya Pasaka, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May aliitisha kikao saa tano mchana na kuahidi kutoa tangazo muhimu.
Wengi walianza kutafakari tangazo lake lingekuwa nini - hadi pale alipotangaza mpango wa kuitisha uchaguzi wa mapema tarehe 8 Juni.
Kulikuwa pia na mzozo kati ya Marekani na Korea Kaskazini ambao umekuwa ukitokota kwa wiki kadha sasa.
Kulikuwa pia na maadhimisho ya uhuru wa Zimbabwe ambapo kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo Robert Mugabe aliwahimiza raia kuutetea na kuulinda uhuru huo.
Nchini Ufaransa, mmoja wa wagombea wakuu katika uchaguzi wa urais Marine le Pen alisema atazuia wahamiaji kuingia nchini humo iwapo atashinda uchaguzi
Siku hizi, BBC ina wafanyakazi wengi na uwezo mkubwa wa kukusanya habari tofauti na hali ilivyokuwa 1930.
Kumekuwa pia na mabadiliko ya maana ya habari.
Wakati huo, habari nyingi zilitoka kwa mashirika ya habari ya kimataifa na matangazo ya serikali.
Siku hizi, watu wa kawaida wanaweza kuwa mada ya habari.
Wakati huo, watangazaji walikuwa pia hawafahamiki na wasikilizaji.
Siku hizi, wengi wa watangazaji wanafahamika sana na hata ni watu mashuhuri.