Google tag

jeudi 4 mai 2017

Aaron Lennon kuugua ugonjwa wa ki Akili

Winga wa klabu ya Everton Aaron Lennon amezuiliwa chini ya kifungu cha polisi cha afya ya kiakili kuhusu wasiwasi wa hali yake.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alipelekewa hospitalini kwa ukaguzi wa kiafya baada ya maafisa wa polisi kuitwa katika eneo la Salford siku ya Jumapili.

Lennon kwa sasa anapata matibabu kwa ugonjwa unaosababishwa na shinikizo la kiakili ,kulingana na klabu hiyo.
Mchezaji huyo wa Uingereza aliyejiunga na Everton kutoka Tottenham 2015 hajachezea kikosi cha kwanza tangu mwezi Januari.

Maafisa wa polisi wa Manchester walisema: Polisi waliitwa saa kumi na nusu mchana kufuatia wasiwasi wa mtu mmoja aliyekuwa katika barabara ya zamani ya eneo la Eccles .
Maafisa wa polisi waliitikia wito huo na mtu mwenye umri wa miaka 30 alikamatwa chini ya kifungu cha 136 cha afya ya kiakili na kupelekwa hositali kwa ukaguzi.

Habari kuhusu kulazwa kwa Lennon zilivutia ujumbe wa kumuombea katika mitandao ya kijamii miongoni mwa wachezaji wa soka na mashabiki wa klabu yake ya zamani na ya sasa.

Conte: Kuna Antonio wawili, na mmoja ni mnyama

Meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte amesema yeye huwa "mnyama" wakati wa mechi, baada yake kushuhudia viongozi hao wa Ligi ya England wakilaza Everton 3-0 Jumapili.

Mwitaliano huyo alisherehekea uwanjani na wachezaji wake baada ya mchezo kumalizika Goodison Park, ambapo mabao yalifungwa na Pedro, Gary Cahill na Willian.

Chelsea wanahitaji kushinda mechi tatu kati ya nne walizosalia nazo msimu huu kushinda taji la ligi, msimu wa kwanza chini ya Conte.
"Kuna Antonio wawili. Ni watu wawili tofauti," alisema Conte, 47.
"Wakati wa mechi, najua kwamba mimi huwa mnyama.

"Baada ya mechi, lazima niwe nimetulia baada yetu kushinda lakini nafikiri ni vyema kusherehekea (ushindi) na wachezaji, wafanyakazi na mashabiki. Hili lina maana kubwa katika maisha yangu."

Conte, ambaye alishinda mataji matatu mtawalia ya ligi ya Serie A akiwa na Juventus kati ya 2012 na 2014, anafahamika sana kwa vituko vyake na nguvu anazoonekana kuwa nazo akielekeza mechi inapokuwa inaendelea.
Alisherehekea mabao ya klabu yake dhidi ya Everton kwa kuruka na kurusha ngumi hewani na kukimbia sehemu inayotengewa wakufunzi nje ya uwanja.
Mwitaliano huyo huwa ametulia wakati wa mahojiano na wanahabari kabla na baada ya mechi, sifa ambazo anasema huwa anapenda wachezaji wake wawe nazo.

"Lazima tuwe na furaha kwa sababu tulicheza mchezo kwa kutumia vichwa vyetu, na kipindi kama hiki katika msimu, ni muhimu kutumia vichwa vyetu, kisha moyo na baadaye miguu," alisema.
Conte anaamini sana kuhusu hilo, kiasi kwamba aliandika kitabu chenye kichwa Testa, cuore e gambe (Kichwa, moyo na miguu) mwaka 2014.

Mechi za Chelsea zilizosalia 2016-17

#Jumatatu, 8 Mei Middlesbrough (Nyumbani)
#Ijumaa, 12 Mei West Brom (Ugenini)
#Jumatatu, 15 Mei Watford (Nyumbani)
#Jumapili, 21 Mei Sunderland (Nyumbani)
#Jumamosi, 27 Mei Arsenal (fainali Kombe la FA)